Binadamu

Binadamu

Binadamu (pia mwanadamu) ni neno lenye asili ya Kiarabu linalomaanisha “Mwana wa Adamu”, anayeaminiwa na dini za Uyahudi, Ukristo na Uislamu kuwa ndiye mtu wa kwanza.

Kisayansi jina hilo linaweza kutumika kwa maana ya Homo sapiens ili kumtofautisha na viumbehai wengine wa jenasi Homo ambao wote walitoweka walau miaka 12,000 hivi iliyopita.

Watu wote walioko leo hii ni spishi ileile na tofauti zinazoonekana kati ya maumbile yao katika sehemu mbalimbali za dunia ni ndogondogo tu.

Utafiti juu ya DNA umethibitisha kwamba binadamu wote wametokana na watu waliokuwepo Afrika walau miaka 300,000 hivi iliyopita.

Kwa namna ya pekee, upimaji wa DNA ya mviringo, ambayo kila mmoja anarithi kwa mama tu, umeonyesha kuwa binadamu wote waliopo duniani wanachanga mama mmoja aliyewahi kuishi miaka 160,000 hivi iliyopita[2].

Halafu upimaji wa kromosomu Y, ambayo kila mwanamume anarithi kwa baba tu, umeonyesha kuwa wanaume wote waliopo duniani wanachanga baba mmoja aliyewahi kuishi walau miaka 120,000 hivi iliyopita[3], kidogo tu kabla ya watu kuanza kuenea katika bara la Asia labda kufuatia pwani za Bahari ya Hindi.

Hata hivyo, miaka hii ya mwisho imegundulika katika baadhi ya wanaume wenye asili ya makabila ya Wabangwa na Wambo (Camerun, Afrika ya Kati) aina ya kromosomu Y tofauti sana na ile ya wanaume wengine wote waliowahi kupimwa, kiasi cha kukadiria zimetofautiana miaka 350,000 hivi iliyopita.

Vilevile, upimaji wa DNA ya mstari kwa jumla umeonyesha uwezekano wa kwamba baadhi ya binadamu wa leo, wale wasio wa Kusini kwa Sahara, wana asilimia 1-6 ya urithi wa kibiolojia kutoka kwa aina nyingine za Homo, hususan Homo neanderthalensis, ile ya pango la Denisova na ile iliyorithiwa na baadhi ya watu wa visiwa vya Andaman (India).

Kama hao waliweza kweli kuzaliana na Homo sapiens na kuacha uzao uliojiendeleza maana yake walikuwa spishi moja na yeye. Hapo asili ya binadamu inatakiwa kuhesabiwa ya zamani zaidi sana kuliko miaka 200,000 iliyofikiriwa kwanza[4].

https://sw.m.wikipedia.org/wiki/Binadamu